Kalonzo: ‘Tutamshinda Ruto debeni, haijalishi atatumia ndumba gani'

Created by Gastone Valusi | | Swahili

Rais Ruto hujieleza kuwa ni mcha Mungu anayejielewa na ambaye lengo lake ni kuona akifanikisha miradi ya maendeleo bila kubagua eneo lolote la nchi kwa misingi ya kikabila.

Muungano wa upinzani utamshinda Rais William Ruto na kumuaibisha vibaya kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, alidai kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, akizungumza mnamo Ijumaa.

Akizungumza katika eneo lake la Ukambani wakati wa hafla ya ugawaji wa vifaa vya uwezeshaji iliyoandaliwa na Gavana Wavinya Ndeti katika Uwanja wa Kenyatta huko Machakos, Bw Musyoka alitangaza kuwa upinzani utamshinda Ruto kwenye kura, “haijalishi ni ndumba gani (Ruto) atakayotumia.”

Licha ya maneno ya Bw Musyoka, ifahamike kwamba Rais Ruto hujisawiri kama mcha Mungu anayejielewa na ambaye lengo lake ni kuona akifanikisha miradi ya maendeleo bila kubagua eneo lolote la nchi kwa misingi ya kikabila.

“Ruto amewekwa kwenye kona. Tumesikia wandani wake wakidokeza kuwa wataleta watu kutoka nchi jirani ili wampigie kura, lakini hata hivyo hatapata idadi hiyo. Sisi katika upinzani ulioungana tumejitolea kutoa mgombea mmoja atakayemenyana na Ruto kwenye kura,” alisema Bw Musyoka.

Akitambua hitaji la kuunganisha kura za eneo la Mashariki ya Chini, Bw Musyoka aliihimiza jamii ya Wakamba kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kama wapiga kura katika shughuli ya uandikishaji wa wapigakura itakayofanywa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

“Ni wakati wa kuikomboa nchi hii. Kuanzia Novemba, IEBC itafanya hatua ya mwisho ya uandikishaji wa wapiga kura, na ninawasihi wote waliohitimu kujisajili watume maombi ya vitambulisho vya kitaifa na wajiandikishe kama wapigakura,” alisema, huku akiapa kwamba atamshinda Dkt Ruto hata katika eneo la Luo Nyanza, iliyokuwa ngome ya aliyekuwa Waziri Mkuu marehemu Raila Odinga.

Bw Musyoka alimshutumu Dkt Ruto kwa kile alichokiita “tabia ya rais ya kutoa ahadi hewa kwa Wakenya.”

“Siku nyingine nilimsikia Ruto akiahidi maelfu ya mabwawa kote nchini. Anapaswa kuja kufanya ukaguzi wa ulinganisho na ulinganuo huku Machakos. Rais mstaafu Hayati Mwai Kibaki na mimi tulipata ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Yatta, na sasa yeye amesalia na miezi kumi ofisini. Atajenga lini?” aliuliza.

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, aliyeambatana na Bw Musyoka, alitangaza kuwa wakati unaisha kwa upinzani kumtambulisha na kumtangaza mpeperushaji wao wa bendera ya urais kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Kiongozi huyo wa chama cha Democratic Party (DP), ambaye ameonekana hadharani akipendelea Bw Musyoka kuwa mgombea wa tiketi ya urais kwa upinzani, alieleza kukata tamaa kwake kutokana na upinzani kusuasua kumtangaza mpeperusha bendera wao.

“Sisi (upinzani) tumechoka kuimba wimbo mmoja kwa miaka mingi kwamba tutamtoa na kumtangaza mtu mmoja wa kumenyana na Ruto. Mtakapotuona hapa siku nyingine, msiruhusu mazungumzo ya namna hiyo. Daini kwamba ni Kalonzo kwa Ikulu,” alisema Bw Muturi.

Wakati wa hafla hiyo, Gavana Ndeti alizindua vifaa mbalimbali vya uwezeshaji vinavyolenga takriban wanufaika 6,000 kote katika kaunti hiyo.

Akihutubia wakazi wakati wa mkutano huo, Bi Ndeti aliwacheka wanasiasa wa mrengo wa United Democratic Alliance (UDA) ambao alidai wamekuwa wakigawa pesa taslimu kwa wananchi, akiita jambo hilo lisilowezekana.

“Ni wakati wa kuwaonyesha wale wanaowakaribia watu wetu kwa kutoa pesa kidogo za mkono kwamba watu wa Machakos wanapopewa zana za kufanya kazi, wanazalisha utajiri wa kweli. Ahadi yangu ni kwamba nitaendelea kutenga rasilimali kwa ajili ya uwezeshaji unaotokana na mali hadi kila kaya huku Machakos ifurahie hadhi ya kiuchumi,” alisema Bi Ndeti.

Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka
Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, akihutubia wafuasi wa chama katika eneo la Ukambani wakati wa hafla ya ugawaji wa vifaa vya uwezeshaji iliyoandaliwa na Gavana Wavinya Ndeti katika Uwanja wa Kenyatta, Machakos mnamo Oktoba 9, 2026. Kalonzo alitangaza kuwa upinzani utamshinda Rais William Ruto katika uchaguzi na kwamba, “haijalishi ni uchawi gani atakaotumia.” Picha/Gastone Valusi>Justice Gauge